1 John 5

Imani Katika Mwana Wa Mungu Huushinda Ulimwengu

1 aKila mtu anayeamini kwamba Isa ndiye Al-Masihi amezaliwa na Mungu, na yeyote ampendaye Baba humpenda pia mtoto aliyezaliwa naye. 2 bHivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu, kwa kumpenda Mungu na kuzitii amri zake. 3 cHuku ndiko kumpenda Mungu, yaani, kuzitii amri zake. Nazo amri zake si nzito. 4 dKwa maana kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, yaani, hiyo imani yetu. 5 eNi nani yule aushindaye ulimwengu? Ni yule tu aaminiye kwamba Isa ni Mwana wa Mungu.

Ushuhuda Kuhusu Mwana Wa Mungu

6 fHuyu ndiye alikuja kwa maji na damu, yaani, Isa Al-Masihi. Hakuja kwa maji peke yake, bali kwa maji na damu. Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli. 7 gKwa maana wako watatu washuhudiao [mbinguni: hao ni Baba, Neno na Roho Mtakatifu. Hawa watatu ni umoja. 8Pia wako mashahidi watatu duniani]: Roho, Maji na Damu; hawa watatu wanakubaliana katika umoja. 9 hKama tunaukubali ushuhuda wa wanadamu, basi ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi, kwa kuwa huu ndio ushuhuda wa Mungu kwamba amemshuhudia Mwanawe. 10 iKila mtu amwaminiye Mwana wa Mungu anao huu ushuhuda moyoni mwake. Kila mtu asiyemwamini Mungu amemfanya yeye kuwa mwongo, kwa sababu hakuamini ushuhuda Mungu alioutoa kuhusu Mwanawe. 11 jHuu ndio ushuhuda: kwamba Mungu ametupa uzima wa milele, nao huo uzima umo katika Mwanawe. 12 kAliye naye Mwana wa Mungu anao uzima, yeye asiye na Mwana wa Mungu hana uzima.

Maneno Ya Mwisho

13 lNawaandikia mambo haya ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu ili mpate kujua ya kuwa mnao uzima wa milele. 14 mHuu ndio ujasiri tulio nao tunapomkaribia Mungu, kwamba kama tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. 15 nNasi kama tunajua atusikia, lolote tuombalo, tunajua ya kwamba tumekwisha kupata zile haja tulizomwomba.

16 oKama mtu akimwona ndugu yake akitenda dhambi isiyo ya mauti, inampasa aombe, naye Mungu atampa uzima mtu huyo. Ninamaanisha wale ambao dhambi yao si ya mauti. Iko dhambi ya mauti, sisemi kwamba utaomba kwa ajili ya hiyo. 17 pJambo lolote lisilo la haki ni dhambi, lakini iko dhambi isiyo ya mauti.

18 qTunajua ya kuwa yeye aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, bali aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hawezi kumdhuru. 19 rSisi twajua kuwa tu watoto wa Mungu na ya kwamba ulimwengu wote uko chini ya utawala wa yule mwovu. 20 sNasi pia twajua ya kwamba Mwana wa Mungu amekuja, naye ametupa sisi ufahamu ili tupate kumjua yeye aliye Kweli. Nasi tumo ndani yake yeye aliye Kweli, yaani, ndani ya Isa Al-Masihi Mwanawe. Yeye ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele.

21 tWatoto wapendwa, jilindeni nafsi zenu kutokana na sanamu. Amen.
Copyright information for SwhKC